Jopokazi linapendekeza mfumo ambao utashughulikia mahitaji yetu ya kipekee, hususan katika kuunda mfumo wa ndani ya nchi au wa kiasili utakaolainisha mamlaka makuu ya nchi na uwakilishi.

 1. Muundo wa mamlaka makuu asilia ya kitaifa - Kuwasikiliza Wakenya kote nchini na kusikia maoni yao kunadhihirisha kuwa wanataka mfumo wa kiasili ambao unaonyesha ujumuishaji katika Mamlaka Makuu, na wakati huohuo wakiwa wanataka kumchagua Rais wao moja kwa moja. Pia waliwaambia Wanajopo kwamba wanataka upinzani wenye mamlaka na Bunge ambalo litawawajibisha wenye Mamlaka Makuu.

 

Muundo wa aina hii una sifa zifuatazo:

 • Kugombea na kushinda Urais - Rais atachaguliwa kupitia haki ya kimsingi ya raia kupiga kura. Ili mgombeaji atangazwe mshindi wa Uchaguzi wa Rais, anapaswa kushinda asilimia 50 + 1 ya kura za Urais na angalau asilimia 25 ya kura zilizopigwa katika kila ya zaidi ya nusu ya Kaunti zote, kama ilivyo sasa.

 • Rais mwenye Mamlaka — Rais atasalia kuwa Kiongozi wa Nchi na Serikali na Amiri Jeshi Mkuu. Yeye atakuwa nembo kuu ya Umoja wa Kitaifa. Rais atakuwa mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri, ambalo linajumuisha Naibu Rais, Waziri Mkuu, na Mawaziri.

 • Kitengo cha Utawala, kwa ruhusa ya Rais, kitakuwa na uwezo wa kuamua sera ya Serikali kwa ujumla, huku Mawaziri, chini ya uongozi wa Waziri Mkuu, watawajibika katika Bunge la Kitaifa kutekeleza shughuli za serikali kwa pamoja.

 • Mihula ya Utawala - Dumisha mihula miwili ya sasa ya utawala kwa cheo cha Urais.

 • Naibu Rais - Naibu Rais ndiye mgombeaji mwenza wa Rais. Yeye ndiye atakayekuwa naibu wa Rais.

 • Waziri Mkuu— Katika muda wa siku maalum zilizowekwa kufuatia kuitishwa kwa Bunge baada ya uchaguzi, Rais atamteua Waziri Mkuu, ambaye atakuwa Mjumbe wa Bunge la Kitaifa aliyechaguliwa kutoka kwa chama cha kisiasa chenye idadi kubwa zaidi ya wabunge katika Bunge la Kitaifa au, ikiwa hakuna chama cha kisiasa chenye wabunge wengi, atateuliwa yule aliye na uungwaji mkono kutoka kwa idadi kubwa ya wabunge.

 • Kuidhinishwa na Bunge — Aliyeteuliwa kwa cheo cha Waziri Mkuu hatachukua mamlaka hadi kwanza uteuzi wake uthibitishwe na azimio la Bunge la Kitaifa linaloungwa mkono na idadi kubwa ya Wabunge.

 • Ikiwa uteuzi wa Waziri Mkuu hautathibitishwa, Rais atachukua idadi fulani ya siku za kuteua mwingine. Utaratibu huu utaendelea hadi pawe na uteuzi wa Waziri Mkuu utakaothibitishwa. Hatua ya kuhakikisha kuwa mchakato huu sio wa kudumu, na kwamba utawala unaendelea unapaswa kuzingatiwa. Jopokazi lingependa pia kusema kwamba baadhi ya raia walionyesha wasiwasi kwamba kukosa idadi kubwa ya wabunge wanaounga mkono uteuzi wa wadhifa huo kunaweza kulemaza ushirikishi katika siasa za Kenya. Kulikuwa na mapendekezo ya kuongeza kiwango na kuhitaji idadi kubwa ya uungwaji mkono. Jopokazi lilihisi kwamba suala hili lilihitaji majadiliano mapana ya kitaifa.

 • Kufutwa kazi— Waziri Mkuu anaweza kufutwa kazi na Rais au kupitia kura ya kutokuwa na imani naye katika Bunge la Kitaifa.

 • Kiongozi Rasmi wa Upinzani— Mwaniaji atakayeibuka wa pili katika uchaguzi wa Urais anakuwa Mbunge ambaye hajachaguliwa na Kiongozi Rasmi wa Upinzani iwapo chama chake hakijawakilishwa katika Serikali, au muungano wa vyama vya Bunge ambavyo havijawakilishwa katika Serikali.

 • Hitaji la kuwa na upinzani wenye nguvu — Chama au muungano wa vyama visivyowakilishwa Serikalini vitakuwa Upinzani Rasmi.

 • Baraza la Mawaziri la Upinzani — Kiongozi Rasmi wa Upinzani atawezeshwa kuteua Baraza la Mawaziri watakaopiga msasa utendakazi wa Serikali katika Bunge. Hii itahusisha uwezo wa kuwa na utafiti bora kuhusu sera na ajenda ya sheria za Serikali.

 • Kipindi cha Maswali — Upinzani utakuwa na jukumu muhimu katika Vikao vya Waziri Mkuu na Mawaziri wakati wa Maswali Bungeni. Kipindi hicho cha Maswali ni fursa kwa Wabunge kuuliza Mawaziri wa Serikali maswali kuhusiana na mambo wanayowajibikia.

    2. Majukumu ya Waziri Mkuu —

 • Waziri Mkuu atakuwa na mamlaka juu ya usimamizi na utekelezwaji wa majukumu na shughuli za kila siku za Serikali.

 • Waziri Mkuu atakuwa Kiongozi wa Shughuli za Serikali katika Bunge la Kitaifa.

 • Waziri Mkuu atajukumiwa na Rais kusimamia kamati ndogo za Baraza la Mawaziri.

 • Katika utumiaji wa mamlaka yake, Waziri Mkuu atafanya au ataelekezwa kufanya jambo au mambo yoyote ambayo Rais ameagiza yafanywe.

 • Waziri Mkuu ataendelea kupata mshahara wake kama Mbunge bila ya mshahara wa ziada kwa majukumu ya uwaziri mkuu.

 • Katibu wa Kudumu/Katibu asiye wa kudumu katika Ofisi ya Waziri Mkuu atasimamia Kamati ya Utekelezaji ya Kiufundi ya Makatibu wa Kudumu/Wasio wa Kudumu.

 • Ili kuondoa siasa katika Utumishi wa Umma, Makatibu Wa Kudumu au Wasio wa kudumu hawataidhinishwa na Bunge. Wajibu wao utakuwa wa kiutawala na kiufundi pekee.

    3. Baraza mseto la mawaziri — Baraza la mawaziri ni sehemu muhimu ya Kitengo cha Utawala wa Serikali. Ukitathmini maoni ambayo Wanajopo walipokea kutoka kwa Wakenya, kuna hali ya kutoridhika na mfumo wa sasa wa baraza hilo. Jopokazi linapendekeza utaratibu ufuatao katika kuunda Baraza la Mawaziri:

 • Rais atateua Mawaziri baada ya kushauriana na Waziri Mkuu. Mawaziri watawajibikia ofisi ambazo Rais atabuni kulingana na Katiba.

 • Baraza la Mawaziri litajumuisha wabunge na wataalamu, watalaamu watafanywa kuwa wabunge ambao hawajachaguliwa baada ya kuidhinishwa na Bunge.

 • Jopokazi pia linapendekeza Waziri aitwe 'Cabinet Minister' badala ya 'Cabinet Secretary'.

 • Ili kuhakikisha kuwa pana mwelekeo mzuri zaidi wa kisiasa na uwajibikaji katika Bunge, kutakuwa na nafasi ya Waziri wa Serikali atakayeteuliwa na wabunge wa Bunge la Kitaifa na kuchukua mwelekeo katika majukumu yao ya uwaziri kutoka kwa Mawaziri. Mawaziri hawa wa Serikali wataendelea kupata mshahara wao kama wabunge bila ya mshahara wa ziada kwa majukumu yao ya uwaziri.

     4. Uwakilishaji

Uwakilishaji katika mfumo wa uchaguzi — Ni muhimu kwamba bila kujali mkondo utakaochukuliwa na mageuzi ya uwakilishaji, yanapaswa kufuata kanuni zifuatazo ikiwa Wakenya watawakilishwa kwa usawa:

 • Kwamba chaguo la watu, kama inavyoonyeshwa katika uchaguzi wa wawakilishi wao, zikiwemo chaguzi ndogo za Vyama na teuzi, litapitishwa kupitia uchaguzi wa haki, huru na wazi.

 •  

 • Watu waliojumuishwa katika orodha yoyote ya Chama watakuwa tayari wamehusishwa kwenye mchakato wa kushiriki mazungumzo ya wazi ya umma katika Kaunti hata kabla ya utaratibu mwingine wowote wa kuwapiga msasa.

 •  

 • Kwamba kutakuwa na usawazishaji katika uwakilishi na usawa wa uraia kadiri iwezekanavyo, kwa kuhakikisha kwamba kila kura ya Mkenya inayo hadhi na nguvu, kama inavyotajwa katika Katiba.

 •  

 • Kupitia kwa Sheria ya Vyama vya Kisiasa, vyama vitalazimishwa kufuata Katiba ili kuafiki Sheria ya Jinsia na sheria nyingine za Katiba zinazohusu ushirikishwaji kupitia orodha ya vyama vyao. Hii itasawazisha jinsia zote mbili katika mahusiko ya kisiasa, badala ya kuunda mfumo sambamba ambao hujenga dhana ya ushirikishi tu.

 •  

 • Orodha ya Madiwani wa chama itafuata kanuni na michakato sawa ya ushiriki wa mijadala ya umma, uchaguzi na kuwapiga msasa kama ilivyo katika Bunge la Kitaifa. Hii itahakikisha kwamba kuna uwajibikaji wa moja kwa moja miongoni mwa watu na vyama.

 •  

 • Maeneobunge yote 290 ya sasa yatahifadhiwa, vikiwemo viti vilivyolindwa kwa sababu vimekuwa vya uwakilishi muhimu wa maeneo ya idadi ndogo ya watu.

 •  

 • Gatua vyama vya siasa ili viwe na matawi imara katika Kaunti na ili viruhusu watu kuwa na vikao vya kisiasa na njia za kuwafanya viongozi waliowachagua wawajibike katika muhula mzima wa uongozi, sio tu wakati wa uchaguzi.

 •  

 • Orodha za uteuzi kupitia kwa vyama zinapaswa kukamilishwa kwa utaratibu wa uwazi unaosimamiwa na vyama vya siasa na kukaguliwa na Msajili wa Vyama vya Kisiasa na IEBC.

Kuna pia mapendekezo ya Jopokazi kuhusu mabadiliko kwa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka. Hii ni pamoja na:

 • Pawe na Utaratibu utakaowapa viongozi wa vyama vya kisiasa bungeni jukumu la kuajiri Makamishna wa IEBC. Katika kufanya uteuzi wa Makamishna, viongozi wa vyama vya kisiasa wanapaswa kuteua watu wasioegemea kokote, walio na rekodi ya ustadi na uadilifu, na wasiojulikana kuwa wafuasi wa kisiasa au wanaharakati wa chama hicho.

 • Kulingana na maoni ambayo Jopokazi lilipokea kutoka kwa Wakenya, imani katika IEBC ingali chini. Kwa hivyo, Jopokazi linapendekeza kwamba pawe na mwanzo mpya tunapoelekea kwenye uchaguzi ujao ili kuimarisha imani ya Wakenya katika taasisi hiyo.

 • Wafanyikazi wote wa IEBC wanapaswa kuajiriwa kwa kandarasi ya miaka mitatu, wanaweza kusaini upya kandarasi nyingine mara moja pekee, ikiwa utendakazi wao ni mzuri. Vinginevyo, itakuwa imetamatika. Hii itazuia kuendeleza makosa kwa kuwezesha kila Tume ifanye uteuzi wakati mmoja katika muhula wake.

 • Maafisa wanaosimamia uchaguzi wanapaswa kuajiriwa kupitia mchakato kama ule unaotumika kuajiri makamishna, ikiwemo kushiriki katika mijadala ya umma. Mwishoni mwa mchakato wa kuajiri maafisa wa kusimamia uchaguzi, IEBC inapaswa kupokea ripoti kuhusu uamuzi waliofanya na sababu zilizowapelekea kufanya uamuzi huo. Hili linapaswa kuwekwa wazi kwa umma.

 • Maafisa wanaosimamia uchaguzi wanapaswa kuwa wakandarasi wa muda na haifai kusimamia uchaguzi mkuu zaidi ya mmoja.

 • Mtu yeyote aliye na uzoefu wa usimamizi wa angalau miaka kumi na mitano (15) katika kiwango cha juu anapaswa kufuzu kuomba nafasi ya kuwa Mwenyekiti wa IEBC. Wadhifa huo haupaswi kutengewa mawakili pekee. Hata hivyo, mmoja wa Makamishna anapaswa kuwa wakili.

 • Maafisa wakuu wote wa sasa wa IEBC wanapaswa kupigwa msasa.

 • Bainisha majukumu ya Katibu na Afisa Mkuu Mtendaji; mfanye Mwenyekiti wa Tume kuwa Afisa Mkuu Mtendaji.

 • Muundo wa Tume lazima uonyeshe Uso wa Kenya katika viwango vyote.

 • Tafiti njia za kutunga vifungu ambavyo vitapunguza gharama kubwa za uchaguzi wetu. Mfumo wa kuunda orodha za vyama ni mojawapo.

 • Fanyia mageuzi mfumo wa sasa wa uchaguzi ili kuhakikisha kuwa ni rahisi, sahihi, wenye kuthibitishwa, salama, ulio na uwajibikaji na wazi kama inavyosisitizwa katika Kifungu cha 86 cha Katiba.