Search

'Huwezi niambia kitu' Utovu wa maadili !

Updated: Mar 24, 2020
Kama walivyonena wahenga, samaki mkunje angali mbichi. Hivyo basi,hatuna budi kuwafunza wadogo wetu maadili wakiwa wangali wachanga ili kuhakikisha taifa linakuza jamii yenye maadili mema na kudhihirisha uongozi wa nchi wenye nidhamu.


Kila uchao, inasikitisha kushuhudia mmomonyoko wa maadili katika jamii yetu. Hili limeathiri sio wale waliokomaa kiumri pekee, bali pia kizazi kinachochipuka kimedhihirisha upungufu mwingi katika kuzingatia nidhamu na maadili. Basi,pasipo budi hubidi, na hatuna budi kurejelea swala la maadili kupitia kufunza maadili shuleni kuanzia kiwango cha chekechea hadi kwenye vyuo vikuu ili kukuza vizazi vyenye nidhamu.


Kuzorota kwa maadili mema kumezidi kuongezeka kitaifa, jambo ambalo limejitokeza wazi katika mfumo wa uongozi wa taifa letu.

Enzi za udogo wangu, swala la maadili lilishamiri na kupewa kipao mbele. Nakumbuka wavyele wangu na majirani walio nizidi umri, siku zote walinipa mwelekeo huku wakinishauri kuwatii wazazi na wale walionizidi umri. VileVile mila, desturi na tamaduni zetu ziliendelea kusisitiza swala hili la maadili na kutoa onyo kali dhidi ya ukiukaji wa maadili. Kutia bidii shuleni, kuamkua watu wazima na kuheshimu wenzangu ni baadhi ya hulka njema ambazo wazazi walifunza wanao.


Kwenye masomo ya chekechea na shule ya msingi pia jambo hili la nidhamu lilizingatiwa kwa umakini na waalimu hawakusita kutuadhibu pale tulipofanya kosa kinyume na maadili mema. Kupitia methali, semi na vitendawili kama vile ‘asiyefunzwa na mamaye hufunzwa na ulimwengu’ vizazi changa viliweza kufanya hima ili kuendeleza heshima na utiifu.


Kupitia simulizi za hadithi bunifu ambazo wahusika wakuu walikuwa wanyama kama vile sungura,simba, fisi n.k walimu waliweza kutuonya dhidi ya tabia zisizofaa. Aghalabu, sungura siku zote alitumika kuonya dhidi ya ujanja huku fisi akitumika kuonya dhidi ya ulafi na tamaa.


Kuzorota kwa maadili mema kumezidi kuongezeka kitaifa, jambo ambalo limejitokeza wazi katika mfumo wa uongozi wa taifa letu. Unyakuzi wa ardhi, ufisadi, unyanyasaji wa wanyonge na wizi wa mali ya uma ni ishara tosha ya ukosefu wa madili. Ukweli na haki vimekosa kutiliwa maanani na hili limepelekea wanyonge kuhisi wamedhulumiwa.


Ni jambo la busara kuhakikisha vizazi tunavyokuza vinazingatia nidhamu na wakati umewadia, sharti kila mmoja atambue kuwa ili kufanikiwa kwa namna yoyote ile, kutia bidii ni njia moja wapo. Njia za mkato kama vile wizi, ufisadi na kujihusisha na mambo ya kikatili ni hulka mbaya ambayo itaibua matokeo mabaya.


Mapendekezo ya jopo la mapatano na maridhiano ya kujenga daraja yanasisitiza umuhimu wa kuwepo kwa mafunzo ya maadili shuleni ili kuendeleza hulka njema na nidhamu. Ni jukumu na wajibu wetu wote kuwa makini zaidi katika kujenga maadili ya kitaifa kutokana na tamaduni tofauti za nchi, masilahi na makundi. Uunganishaji amali za kitamaduni na kaida za kisasa za wakenya kama inavyoonyeshwa katika sherehe za kitamaduni za kuingia utuuzima na maadili na kanuni za Katiba, na Majukumu na Haki za uraia ni mbinu mojawapo itakayo changia katika kuendeleza maadili.

351 views2 comments

© 2020 Building Bridges Initiative 

bbi@citizensupport.go.ke

Join The Conversation #BBIReport

  • Facebook
  • Twitter