Search

Je, Wamkumbuka Jaji Lucy wa Vioja Mahakamani?

Updated: Feb 5, 2020Kwa zaidi ya miongo miwili, Lucy Wangui aliigiza kama jaji wa mahakama katika kipindi cha Vioja Mahakamani ambacho kilipendwa na kuenziwa na wakenya wengi. Japo watu wengi walikuwa hawajapata fursa ya kuingia mahakamani wala kuelewa jinsi shughli mahakamani huendeshwa, kipindi hiki kilidhihirisha taswira ya taratibu za mambo yanavyotukia kotini.


Licha ya kuwa ni uigizaji tu, Lucy siku zote alionekana mwanamke shupavu na jasiri katika kufanya maamuzi ya visa tofauti kama vile vya mauwaji, vita, ulaji rushwa, hatia za barabarani kama vile uendeshaji gari mbaya, unyanyasaji na kadhalika. Bila shaka, watu walishuhudia sura kamili ya jaji wa mahakama kupitia kwa uigizaji Lucy Wangui.


Bila ubaguzi wala kuegemea upande wowote, Lucy alifanya maamuzi ya matukio mbalimbali kwa haki na ukweli.

Kupitia kuupa upande wa mashtaka nafasi ya kujieleza na kujitetea na upande wa mashahidi kuweza kutoa kauli yao, jaji huyo aliweza kusikiliza pande zote kwa makini na mwishoni kufanya maamuzi ambayo yangepelekea mshtakiwa kufungwa iwapo angepatikana na kosa au kuachiliwa huru ikiwa hana kosa.


Nchini Kenya, idara ya mahakama imekuwa ikishuhudia changamoto si haba na wakenya wengi kupitia vyombo vya habari na mitandao wamekuwa wakionyesha hisia za kughadhabishwa na matukio mbalimbali, ambayo yanadhihirisha ukosefu wa Imani kwa mahakama. Aghalabu kumekuwepo na tetesi kuwa baadhi ya matukio huchukua muda mwingi kuamuliwa na hata kesi zingine kukosa kupewa uzito, jambo ambalo limeonyesha hali ya kutowajibika upande wa mahakama.


Mahakama imeonekana kuwa miongoni mwa taasisi zenye ufisadi mwingi nchini. Mara kwa mara kumekuwepo malalamishi yanayoonyesha kuwa kesi zingine zimetupiliwa mbali kwa misingi ya ulaji rushwa. Vilevile ubaguzi umejitokeza wazi pale ambapo jamii masikini na wanyonge wasioweza kutoa kiwango fulani cha hela huhukumiwa na kufungwa mara moja kwa makosa madogo kama vile wizi, vita na unywaji pombe haramu, ilhali mabwenyenye huwachiliwa huru kwa makosa kama vile mauwaji, ufisadi, jinai, unyakuzi wa ardhi ya umma na kadhalika. Mrundikano wa kesi mahakamani limekuwa tatizo kuu. Hili linajitokeza wazi kwani tunashuhudia kesi za miaka mingi iliyopita ingalipo bila uamuzi kamili kupatikana.


Kama vile uigizaji wa jaji Lucy, mahakama humu nchini inahitaji mabadiliko yatakayoipa sura mpya. Uwazi na uwajibikaji ni vipengele muhimu katika kuipa mahakama yetu taswira mpya na kuhakikisha kesi zinahukumiwa kwa haki na ukweli.

Kwa kuiga mfano mwema wa Jaji Mwigizaji Lucy, mahakama ya Kenya inafaa kushughulikia kesi mbalimbali bila ubaguzi wala kuegemea upande wowote. Kuwepo na sheria itakayolinda haki za wanyonge kutadhihriisha usawa na haki mahakamani na wanyonge hawatahisi kudhulumiwa.


Ili kukabiliana na kusuluhisha matitizo yanayoikumba mahakama, jopokazi la maridhiano ya kujenga daraja -BBI linatoa pendekezo la kuzidisha imani ya raia kwa idara ya mahakama kwa kutambua kuwa mihimili mikuu ya katiba nchini Kenya ni kutenganisha mamlaka kati ya vitengo vikuu vya serikali na uwajibikaji kwa wakenya. Ni sharti uhuru wa mahakama ulindwe kama mhimili mkuu, lakini nayo pia inapaswa kuwajibikia wakenya.


Mahakama ikiiga mfano unaotolewa na jaji Lucy Wangui kwa kufanya kazi kwa ukweli na uwazi bila ubaguzi wala upokeaji hongo, mtizamo wa wakenya utabadilika na Imani yao kwa mahakama kuongezeka.

173 views0 comments

© 2020 Building Bridges Initiative 

bbi@citizensupport.go.ke

Join The Conversation #BBIReport

  • Facebook
  • Twitter