Search

Mfumo wa Uongozi wa Utotoni na wa Kisasa (Hadithi ya Ugatuzi)


Ni jioni yenye utulivu, siku ya Ijumaa, nimeketi kivulini napunga hewa nyumbani huku nikiwaza na kuwazua… Je, ni kipi kipya kimejiri tangu enzi za utotoni?


Naam, kadri miaka inavyozidi kusonga, ndivyo mambo yanavyozidi kubadilika. Kama mzaliwa wa eneo hili la Elgeyo Marakwet, nafahamu fika kuwa, kumbukumbu ni hazina isiyoweza kuibika na kipindi hiki cha tafakari ni dhihirisho bayana kuwa yapo mabadiliko mengi yameshuhudiwa kwa muda wa miaka saba iliyopita hususan katika eneo hili.

Kwa zaidi ya miaka kumi na moja, tangu safari yangu ya elimu ya chekechea kung’oa nanga hadi nilipokamilisha masomo ya kidato cha nne mwaka elfu mbili na tisa, hali ilikuwa si hali kwani tulikuwa tumeyazoa maisha yenye changamoto si haba. Kila kukicha matatizo yalibakia kuwa ni yale yale. Umasikini, upweke na ufukara ni matatizo yaliyowakumba wengi katika makaazi yetu.


Nyumbani, maisha yalizidi kuwa magumu huku tukishuhudia uhaba kifedha, jambo ambalo lilipelekea wazazi wangu kuhama kutoka eneo moja hadi lingine kila mara

Kiuchumi, hali ilizidi kuzorota na kudidimia pasi na dalili yoyote ya maendeleo. Barabara mbovu zisizoweza kupitika, kukosa ajira, ukosefu wa shule na hospitali, ukulima usioleta faida kifedha na kadhalika ndiyo mazingira yaliyotuzunguka siku zote tusione tumaini. Nyumbani, maisha yalizidi kuwa magumu huku tukishuhudia uhaba kifedha, jambo ambalo lilipelekea wazazi wangu kuhama kutoka eneo moja hadi lingine kila mara kwa kutafuta nafasi za ajira duni ili kukidhi mahitaji ya kimsingi ambayo ni chakula, makao na karo ya kutuendeleza kielimu. Hali hii iliashiria si maisha ya wakaazi wa Elgeyo Marakwet pekee bali pia ya wakaazi wa maeneo mengi haswa yale ya mashinani nchini Kenya ambayo yako mbali na miji mikuu.


Muda huu wote, hakuna yeyote aliyekuwa na uwezo wa kufahamu kuwa hatimaye matumaini yangeibuka kupitia uzinduzi wa mfumo wa serikali za majimbo, kama ilivyokuwa ndoto ya waanzilishi na wapiganiaji uhuru wa taifa letu la Kenya kutoka kwa uongozi wa ubeberu.


Hayawi hayawi huwa! Ni takriban miaka saba tangu kuanzishwa kwa serikali za majimbo ambapo serikali 47 za ugatuzi zilizinduliwa kutokana na kupitishwa kwa katiba mpya ya 2010. Mfumo huu wa ugatuzi uliibua uhamishaji wa majukumu kutoka serikali ya kitaifa hadi serikali za majimbo. Uongozi huu, umewapa wakenya wengi hususan wanaoishi mashinani matumaini mengi.


Licha ya changamoto kadha zinazokumba ugatuzi, leo hii kama mwandishi kutoka Elgeyo Marakwet, ninajivunia na kuionea fahari nchi yangu ya Kenya haswa eneo langu la kuzaliwa kwani kupitia ugatuzi nafasi za ajira zimeongezeka.

Hii ni kutokana na miradi mingi ambayo imeanzishwa kupitia uongozi wa kaunti. Kuwepo kwa miundombinu na vifaa vifaavyo kumezua maendeleo mengi kiuchumi. Vituo vya afya, shule na barabara ni baadhi ya matunda tunayoshuhudia kutokana na ugatuzi. Wakulima, wakiwemo wavyele wangu wanatabasamu kwa kupata mafunzo kabambe yatakayo hakikisha wamepata faida kupitia uzinduzi wa soko la mazao ya mashamba na kujihusisha na kilimo biashara.


Kwa hakika ugatuzi haubagui miji, vijiji wala vitongoji.Mapinduzi ya kiuchumi, yameibua uzalishaji utakaowafaidi wakenya wote.

262 views0 comments

© 2020 Building Bridges Initiative 

bbi@citizensupport.go.ke

Join The Conversation #BBIReport

  • Facebook
  • Twitter