1. Dumisha kaunti zote 47 lakini himiza na usaidie kaunti kuunda, kwa hiari, maeneo ya kiuchumi.

 2. Ongeza pesa katika kaunti kwa angalau asilima 35 ya akaunti za mwisho zilizofanyiwa mahesabu.

 3. Wakati wa kutenga pesa katika kaunti, tumia fomula inayolenga kuhakikisha kwamba huduma zinafikia maeneo ya wakazi halisi ili pesa zisitolewe kwa misingi ya ukubwa wa eneo.

 4. Kamilisha uhamishaji wa majukumu kutoka Serikali ya Kitaifa hadi Serikali za Kaunti na ondoa urudiaji wote wa majukumu kati ya ngazi hizo mbili za serikali.

 5. Fuata usemi "pesa hufuata majukumu" katika kutenga pesa kati ya ngazi mbili za serikali.

 6. Zingatia jinsi Wawakilishi wa Wadi wanavyoweza kusimamia fedha za basari pekee, huku wakihakikisha kuwa hakuna mgongano kati ya matumizi ya fedha za CDF na fedha za kaunti katika maendeleo ya Kaunti.

 7. Mabadiliko katika Usimamizi wa Kaunti —

  • Iwapo nafasi ya Naibu Gavana itakuwa wazi kwa sababu zozote zile, kisha Gavana akose kuteua naibu kwa muda wa siku 90, basi Spika wa Bunge la Kaunti atateua Naibu Gavana kwa idhini ya bunge la kaunti.

  • Mgombea mwenza wa yule anayewania ugavana hawezi kuwa wa jinsia moja naye. (Gavana akiwa wa kiume, naibu wake ni wa kike).

 8. Tume ya Huduma za Afya - Hamisha wafanyikazi katika sekta ya afya kutoka serikali za kaunti hadi Tume huru ya Huduma za Afya ili kuweza kugawana wataalamu wa afya walio wachache.

 9. Gharama za usimamizi wa Bima ya Kitaifa ya Afya (NHIF) zinapaswa kupunguzwa zaidi kwa kutumia teknolojia, kupunguza visa vya ufisadi na kuongeza tija. Gharama hizi za kiusimamizi zinapaswa kuwa kati ya 5 na 10.

 10. Kuandaa na kupitisha mswada wa haki za mgonjwa ili kusawazisha ubora wa huduma za afya katika kaunti zote.

 11. Matumizi ya Pesa katika Serikali za Kaunti - Usimamizi wa Matumizi ya Pesa katika Kaunti, uwekezaji na utoaji wa nafasi za kazi havifanikiwi katika viwango vingi, hali inayosababisha ubadhirifu mkubwa wa pesa na ufisadi ambao unatatiza ugatuzi. Ufisadi ni janga ambalo ni maarufu sana kwa Wakenya. Ni muhimu pia kwamba uangalizi wa pesa hizo unaimarishwa.

  • Jibu linapaswa kuwa uangalizi wa pesa ulioimarishwa na mashirika husika, hatua za kupunguza ubadhirifu, na kutenga sehemu kubwa ya fedha za Kaunti kwa maendeleo.

  • Kufadhili maendeleo ya kila Wadi kwa hadi asilimia 30 ya bajeti ya maendeleo ya Kaunti katika kipindi cha miaka mitano.

  • Uwiano kati ya matumizi ya fedha za maendeleo na matumizi ya kawaida unapaswa kuwiana na ile ya kitaifa kwa 70:30.

  • Kuimarisha uhuru wa Mabunge ya Kaunti ya uangalizi wa fedha kwa kuhakikisha kuwa upitishaji na usimamizi wa bajeti za Bunge la Kaunti unalindwa kutokana na kuingiliwa kiholela au kisiasa na Maafisa Wakuu wa Kaunti; michakato hii inapaswa pia kupigwa msasa mkali na usimamizi wa fedha za umma.

  • Hitaji la serikali mpya kukamilisha miradi iliyoanzishwa na magavana wa zamani na Hazina ya Kitaifa kuzuia fedha za miradi mpya hadi ile ya zamani ikamilike. Ni sharti gavana ambaye anataka kuachana na mradi wa zamani awasiliane rasmi na umma akitoa sababu mwafaka za kufanya hivyo.

 12. Kaunti pia zipanue mawanda ya vitega-uchumi — Kaunti zinapaswa kuongozwa na lengo kuu la kuvutia wakazi wake zaidi katika ujasiriamali, na uwekezaji kutoka sehemu nyinginezo za nchi, na nje ya nchi, uelekezwe kwenye Kaunti.

 • Katikati ya haya ni kwamba udhibiti na ukusanyaji wa mapato unaofanywa na Serikali ya Kaunti usivuruge vivutio vya uwekezaji na ubunifu.

 • Biashara mashinani — Ni lazima kila Kaunti ifanye juhudi kubwa za kimakusudi kusaidia makundi ya wenyeji ili kukuza biashara kupitia ushirika. Serikali ya Kaunti inapaswa kuhakikisha kuwa kuna utaratibu mwepesi wa kuanza biashara ndogondogo na zile zinazoanza, na kwamba ni rahisi kwa wafanyabiashara kufuata kanuni na urasimu, huku bidhaa zao zikifika sokoni kwa wakati unaofaa.

 • Kila Kaunti ianzishe na kutangaza Kanuni ya Ujasiriamali na Uwekezaji ambayo itaitumia kwa njia inayotabirika na thabiti.

 • Hata ingawa Kaunti zinainua mapato yake, ni lazima zidhibiti ufujaji zikijua fika kwamba zinashindana si tu na Kaunti nyingine nchini lakini pia na nchi nyinginezo na majimbo yazo.

13 .Hakuna kutoza ushuru mara mbili na pia hakuna sheria mbili za ushuru katika ngazi ya Kitaifa na Kaunti — Taratibu za serikali na serikali nyingine zinapaswa kuundwa na kubainishwa ili kuhakikisha kuwa lengo hili linatimizwa kila wakati.

14. Kaunti zenye utangamano zaidi — Kuimarisha mazungumzo na mshikamano wa kijamii katika Kaunti, hususan kaunti ambazo zina makabila mengi, kwa lengo la kuhakikisha kuwa jamii zenye idadi ndogo ya watu zinasikika na kuheshimiwa.