Wakenya waliambia Wanajopo kwamba hawajisikii salama. Jopokazi lilibaini kwamba Kenya iko katika eneo hatari na vitisho vya ugaidi vinavyozidi kujitokeza, mataifa yenye utawala unaoyumba au dhaifu na nchi zenye mizozo ya kimipaka, unyanyasaji wa polisi na matendo haramu ya kijambazi yanayokiuka haki za binadamu. Jopokazi linapendekeza hatua madhubuti zifuatazo:

 1. Sawazisha thamani ya maisha ya Mkenya katika kila sehemu ya nchi -Thamani ya maisha iliyoathiriwa na vurugu, ukosefu wa usalama na viwango duni vya usalama inapaswa kuwa sawa kote Kenya. Ni sharti tuache mazoea ya dhana kwamba kuna matokeo tofauti ya vurugu katika sehemu tofauti ya nchi. Kufanya mabadiliko haya kunahitaji usawa katika usambazaji wa maafisa wa polisi, mashtaka na juhudi za kuzuia uhalifu.

 2. Mkakati wa Usalama wa Kitaifa unaojivuniwa na raia — Baada ya kugundua kuwa usalama ni wa raia, tunahitaji mbinu inayozingatia usalama wa kibinadamu iwekwe katika Mkakati kamili wa Kitaifa wa Usalama na Ulinzi (kila baada ya miaka miwili na kila Rais anayeingia mamlakani katika kipindi cha miezi mitatu baada ya kuchukua hatamu za uongozi) na ambayo inamilikiwa na watu na serikali yote. Inapaswa kuwa amilifu, yenye kuzuia, na ya kutahadharisha.

 3. Kutoathiriwa sana na migogoro ya rasilimali, majanga, dharura na uhaba wa chakula kwa kutekeleza Mkakati kamili wa Dharura za Kitaifa, Mkakati wa Kushughulikia Maafa na Migogoro uliowekwa kwenye sheria ambayo inahusishwa na mipango ya kukabiliana na majanga katika ngazi ya kaunti, kaunti ndogo na wadi ambayo husasishwa mara kwa mara.

 4. Ugaidi ni tishio linaloendelea kuathiri Wakenya ambao wanahitaji zana mbalimbali kulishughulikia, si usalama tu - Kukabiliana na Ugaidi kutafanikiwa tu ikiwa utahusishwa zaidi na ulinzi wa kisiasa, kijamii na kitamaduni ambao hupunguza idadi ya wanaosajiliwa, na kutohalalisha malengo ya maadui wetu.

  • Kuangazia na kuratibisha mipango ya kuzuia itikadi kali na mafunzo yanayochochea vurugu katika Wizara zinazohusika na afya, elimu, vijana, utamaduni na turathi.

  • Kuhusu namna Fedha za Kulinda Waathiriwa zinavyotumiwa, waathiriwa wa ugaidi wanapaswa kupewa kipaumbele kwa kuwa kunyanyaswa kwao kunalenga kutishia Wakenya wote moja kwa moja pamoja na viongozi tuliochagua kwa misingi ya kisiasa, kijamii na kidini.

 5. Masuala ya Kigeni— Kutathmini mahusiano ya kidiplomasia na mataifa yanayofadhili ugaidi, misimamo mikali ya kidini, na upanuzi au kujitenga Hakikisha diplomasia imeundwa na kufadhiliwa ili kukabiliana na vitisho vinavyoibuka kabla ya kudai mwitiko madhubuti wa usalama. Kuhusiana na bajeti, ni muhimu kwamba Wizara ya Masuala ya nje, inapata mgao sawa na Idara ya Ulinzi, Huduma ya Kitaifa ya Ujasusi (NIS), na vyombo vingine vya usalama.

 6. Utendakazi wa polisi, na afya ya akili na ustawi - Kuimarisha utendakazi na huduma za Shirika la Huduma za Kitaifa za Polisi, pamoja na kuboresha afya ya akili na ustawi wa maafisa hao.

  • Fafanua Viashiria Muhimu vya Utendakazi kwa makamanda wa polisi kutoka katika ngazi ya Inspekta Jenerali wa Polisi hadi chini kwa kitengo cha umma cha kuripoti takwimu za uhalifu wa kitaifa na ukosefu wa usalama. Vitengo hivi viwili vizingatiwe katika kupandisha vyeo na kutoa vivutio.

  • Unga mkono maadili na utendakazi bora katika NPS kwa kutambua na kutuza ufanisi, kujituma na kujitolea kwa maafisa na wananchi.

  • Kama suala la kipaumbele, pawe na huduma za ushauri kuhusu afya na matibabu ya akili ya maafisa wa polisi. Polisi walio na majukumu makubwa ambayo yanawaweka katika hatari ya kudhurika kiakili wapewe mazingatio maalum. Hatua zote zinapaswa pia kuchukuliwa ili kuweka familia pamoja.

 7. Linda Wananchi dhidi ya vitisho vya kibinafsi na hatari

  • Kukabiliana na visa vya unyanyasaji wa kijinsia na ngono kupewe kipaumbele kwa kuzingatia na kutoa rasilimali maalum kwa polisi na kuchukua hatua za kuzuia dhuluma za kijinsia na ngono.

  • Shughulikia mizozo ya mipaka ambayo inahatarisha usalama wa kitaifa na jamii - Unda tume maalum au majopokazi kwa kila mzozo wa mpaka ili washauriane na wadau wote na kutoa mapendekezo ya mageuzi ambayo yatashughulikiwa.

  • Wafichuzi wa uhalifu walindwe — Wezesha taratibu za mahakama ambazo zitahakikisha usalama na ulinzi wa watoaji habari, wafichuzi na mashahidi, hususan wa ugaidi, uhalifu mkubwa wa kimataifa, na ufisadi.

  • Utatuzi wa migogoro inayokumba wananchi - Imarisha ujuzi wa raia wa kutatua migogoro na upatanishi katika mfumo mzima wa elimu ya Kenya. Fanikisha hili kwa kujumuisha maarifa ya utatuzi wa migogoro, mazungumzo na ushauri katika mtaala wa elimu katika ngazi zote za elimu ya msingi na sekondari.

  • Linda Wakenya dhidi ya vyakula hatari kwa kuimarisha usimamizi wa usalama wa chakula.